BI. MEENA ARIDHISWA NA SHUGHULI ZA UZALISHAJI MBEGU BORA ZA MIFUGO NAIC


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Kisaka Meena ameridhishwa na shughuli za Uzalishaji wa mbegu Bora za ng'ombe bora, ambazo uzalishwa kwa njia ya kisasa zaidi na ya kiteknolojia ya juu zaidi ili kuwapatia wafugaji mbegu iliyo Bora zaidi.


Akizungumza leo Aprili 28, 2026 Jijini Arusha kwa Niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo Kanda ya Kaskazini (ZVC) na Kituo Cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), Bi. Meena amesema kuwa yeye amekuwa shuhuda na ameona kazi zinazofanywa na Kituo cha NAIC pamoja na jitihada zinazofanyika katika kuzalisha mbegu Bora za Mifugo.


"Serikali iliweka Kituo hiki kwa lengo la kuzalisha Mbegu Bora za Mifugo ambazo zitawasaidia wafugaji kupata mbegu hizo kiurahisi zaidi na kwa bei nafuu." amesema Bi. Meena


Aidha, Bi. Meena, amewataka wafugaji kuendelea kutumia mbegu Bora zinazozalishwa na Kituo cha NAIC ili kuweza kuboresha zaidi Mifugo yao na hatimae kuingia kwenye Masoko ya nje ili kuweza kujiongezea kipato zaidi kutokana na fedha za kigeni.


Vilevile, Bi. Meena ameitaka ZVC Kanda ya Kaskazini kuendelea kuzitumia Dozi za chanjo zilizopo ili kuweza kuwahudumia wafugaji na Mifugo yao kwa lengo kutokomeza magonjwa mbalimbali ya Mifugo ikiwemo ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo.


Pia, Bi. Meena amebainisha changamoto mbalimbali alizozisikia kutoka katika Vituo hivyo viwili, na kuweka wazi kuwa Wizara itaanza zifanyia kazi ili kuweza kuhakikisha Vituo hivyo vinakuwa Bora zaidi na kutoa Huduma ipasavyo kwa wafugaji na Mifugo yao.


Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa NAIC, Dkt. Dafay Bura, ameweka wazi kuwa NAIC inaendelea kutoa elimu kwa wafugaji ili waweze kujua umuhimu wa kuwa na mbegu Bora ya ng'ombe ili kuleta tija katika Mifugo yao.


Naye, Kaimu Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo Kanda ya Kaskazini (ZVC) Arusha, Dkt. Robert Buluba, ameweka wazi Mikakati ya Kituo hicho katika kuboresha Huduma Bora za Mifugo, ikiwemo kuendelea kufanya Uchunguzi zaidi wa magonjwa na kuwapatia wafugaji Chanjo ambazo zitasaidia katika kutokomeza magonjwa ya Mifugo.






No comments