MHE. SANGU AWAASA WAAJIRI KUZINGATIA SHERIA ZA AFYA NA USALAMA MAHALA PA KAZI


 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Deus Sangu, ameongoza kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi Duniani yaliyofanyika mkoani Njombe, akitoa wito kwa waajiri na wafanyakazi kuweka kipaumbele ustawi wa wafanyakazi na mazingira salama ya kazi.


Akizungumza jana Aprili 28, 2026 katika kilele cha Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Mhe. Sangu amewakumbusha waajiri wote nchini kutekeleza wajibu wao wa kisheria, ikiwemo kusajili maeneo ya kazi katika Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) na kutoa taarifa za ajali zitokeazo kazini kwa mujibu wa sheria.


“Ninatoa rai kwa waajiri wote ambao bado hawajasajili maeneo yao ya kazi OSHA kufanya hivyo mara moja kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema.


Ameeleza kuwa usalama na afya kazini ni msingi muhimu wa kuongeza uzalishaji, kulinda nguvu kazi ya taifa na kuchochea maendeleo endelevu. Hivyo, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya usalama kazini, ikiwemo utoaji wa vifaa vya kujikinga, mafunzo endelevu kwa wafanyakazi na uboreshaji wa mazingira ya kazi ili kupunguza ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.


Mhe. Sangu amewata wafanyakazi kuwa mstari wa mbele kufuata taratibu za usalama, kutumia ipasavyo vifaa kinga wanavyopewa na kutoa taarifa mapema kuhusu vihatarishi vinavyoweza kusababisha madhara kazini.


Maadhimisho hayo yamewakutanisha viongozi wa Serikali, waajiri, wafanyakazi na taasisi mbalimbali, yakipambwa na matembezi ya pamoja, maonesho na utoaji wa elimu kuhusu afya na usalama kazini, kwa lengo la kuhamasisha mazingira salama na yenye tija.


Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) nalo limeshiriki kikamilifu katika maonesho hayo yaliyofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 28 Aprili, 2026, yakiongozwa na kaulimbiu: “Mazingira bora ya kisaikolojia na kijamii kazini ni njia ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kujenga taasisi imara.”







No comments