BILIONI 18.29 ZATUMIKA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA VYOO SHULE ZA MSINGI, SEKONDARI
Serikali imetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 18.29 kujenga matundu ya vyoo 6, 283 kote nchini, katika mwaka wa fedha 2024/2025 na 2025/26 hadi kufikia mwezi Aprili, ili kukabiliana na uhaba wa vyoo katika shule za msingi na sekondari nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange kwa Niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara leo Aprili 27, 2026, Bungeni jijini Dodoma, aliyetaka kufahamu Serikali imejipangaje kumaliza tatizo la matundu ya vyoo katika halmashauri nchini.
Dkt. Dugange ameeleza kuwa Serikali imekuwa ikifanya tathmini ya kila mwaka ili kubaini mahitaji halisi ya matundu ya vyoo kulingana na ongezeko la wanafunzi. Takwimu za Sensa ya Elimu Msingi ya mwaka 2025 zimeonyesha kuwa kwa sasa uwiano wa matundu ya vyoo ni tundu moja kwa wanafunzi 46 wa kiume na 42 wa kike kwa shule za msingi, huku sekondari hali ikiwa ni tundu moja kwa wavulana 27 na wasichana 25.
Katika kutekeleza hilo amesema, Serikali imetumia kiasi cha Shilingi Bilioni 12.87 kwa mwaka wa fedha 2024/25 kujenga matundu ya vyoo 6,283 kote nchini. Aidha, kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 hadi kufikia mwezi Aprili 2026, kiasi kingine cha Shilingi Bilioni 5.42 kimetolewa kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa idadi hiyo hiyo ya matundu ya vyoo ili kupunguza pengo la uhitaji uliopo.
"Zoezi hili ni endelevu kwa sababu tutaendelea kujenga shule, idadi ya watoto itaendelea kuongezeka. Kwa hiyo hakuna siku tutasema tumemaliza, shule zitaendelea kujengwa na zitahitaji kujenga vyoo." amefafanua Dkt. Dugange.
Vilevile, ameeleza kuwa Serikali imeweka dhamira ya dhati ya kuondokana na changamoto hiyo kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri na fedha kutoka Serikali Kuu. Amesema kuwa tathmini ya hivi karibuni imependekeza kuwa shule yenye wanafunzi 400 inahitaji wastani wa matundu ya vyoo 12, huku baadhi ya shule nchini zikiwa tayari zimevuka kiwango hicho cha ubora.
Dkt. Dugange amemhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imejipanga vizuri katika kutenga bajeti kila mwaka ili kuhakikisha shule zote nchini zinakuwa na miundombinu inayojitosheleza.
Post a Comment