BUNGE LAPITISHA BAJETI YA WIZARA YA NISHATI YA SH TRILIONI 2.53.


BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha kwa kishindo shilingi trilioni 2.53 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati 2026/2027.

Kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 2.46 sawa na asilimia 97.5 ya bajeti yote  imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na asilimia 2.5 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.


Akihitimisha hoja kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2026/2027 Waziri wa Nishati,Deogratius Ndejembi, amelieleza Bunge kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kuhakikisha kwamba maono ya Rais,Dkt. Samia Suluhu Hassan, maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi na mwelekeo uliowekwa kwenye Dira 2050 yanatekelezwa kwa vitendo na kwa haraka.


Kutokana na hilo ameeleza kuwa lengo lililowekwa kwa Wizara la kuzalisha umeme  wa megawati 8000 ifikapo 2030 litatekelezwa kwani Wizara ya Nishati imeshajipanga kuzalisha kiasi hicho cha umeme huku ikidhamiria kuzalisha megawati 70,000 ifikapo 2050.


"Ili kutekeleza lengo hili tutatumia vyanzo vyote vinavyopatikana kwenye Taifa letu ikiwemo vyanzo vya maji kama vile Malagarasi (49.5MW), Kakono (87MW), Ruhudji (358), Rumakali (222MW),  Jeothemo na makaa ya mawe.." Alisema Mhe. Ndejembi


Akifafanua uhusu mradi wa uzalishaji wa umeme wa makaa ya mawe Waziri Ndejembi amesema Tanzania ina hifadhi kubwa ya makaa hayo na sasa Serikali inashirikiana na Sekta binafsi ili kuhakikisha kuwa inaanza uzalishaji wa megawati zaidi ya 2000 kwa kutumia nishati hiyo.






No comments