CHUO CHA KODI (ITA), WADAU WAKUTANA KUJADILI MTAALA WA SHAHADA YA UZAMILI YA FORODHA NA BIASHARA ZA KIMATAIFA


Chuo cha Kodi (ITA) na wadau mbalimbali wamekutana Chuo cha Kodi katika warsha kujadili mtaala wa kozi ya Shahada ya Forodha na Biashara za Kimataifa ambayo Chuo kinatarajia kuanzisha.


Akizungumza wakati wa kufungua warsha hiyo, Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo amesema Chuo kinatarajia kuanzisha Shahada ya Uzamili katika Forodha na Biashara za Kimataifa na Shahada ya Sayansi ya Kodi hivyo kinahitaji mchango kutoka kwa wadau ili kuwa na mtaala ambao umeegemea katika mafunzo ya umahiri.


“Tumewaalika wataalamu wa forodha na biashara ya kimataifa kuhakikisha kwamba programu hii inakidhi mahitaji ya kisasa na inalingana na viwango vya kitaifa na vya kimataifa,” alisema Prof. Jairo.


Prof. Jairo aliongeza kuwa Shahada ya Uzamili ya Forodha na Biashara za Kimataifa inalenga kuwajengea watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wadau wengine ujuzi wa kushughulikia changamoto za kisasa katika sekta ya forodha na biashara za kimataifa. Aidha, alisisitiza kuwa mtaala huo utazingatia mfumo wa Elimu na Mafunzo unaozingatia Umahiri (CBET) na mahitaji ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Wizara husika za Serikali pamoja na mashirika ya kikanda na kimataifa kama Shirika la Forodha Duniani (WCO), Shirika la Biashara Duniani (WTO), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).


Alibainisha pia kuwa programu hiyo itakuwa ya kipekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini kwa kuwa hakuna shahada ya aina hiyo Tanzania na pia katika ukanda huo. “Ushiriki wenu ni muhimu ili kuhakikisha tunapata mtaala wa vitendo na wenye tija kwa taifa,” alihitimisha.



Warsha hiyo ilihudhuriwa na wadau kutoka taasisi na mashirika mbalimbali, ambapo washiriki walihimizwa kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha mtaala unaopatikana unakuwa bora na unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.







No comments