SERIKALI KUIMARISHA HUDUMA ZA USINGIZI NA GANZI KUPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO


Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi amesema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za dawa za usingizi tiba na ganzi salama ili kuboresha usalama wa upasuaji na kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga nchini.


Dkt. Samizi amesema hayo kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa katika Kongamano la nne la Kisayansi la Chama cha Wataalam wa Dawa za Usingizi na Ganzi Tanzania, Aprili 22, 2026 jijini Dodoma.


Dkt. Samizi amesema wataalamu hao ni muhimili muhimu katika kuhakikisha huduma salama za upasuaji zinapatikana nchini.


Amesema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya afya, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa vituo vya kutolea huduma za afya vyenye vyumba vya upasuaji ili kusogeza huduma karibu na wananchi.


Dkt. Samizi amewapongeza wataalamu wa usingizi na ganzi kwa mchango wao mkubwa katika utoaji wa huduma za afya, akibainisha kuwa taaluma hiyo ina nafasi ya kipekee katika kuhakikisha upasuaji unafanyika kwa usalama na ufanisi.


Amesema kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kujadili changamoto zinazoikabili taaluma hiyo pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha huduma, hususan katika kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.


Aidha, ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mafunzo ya taaluma hiyo kwa kuimarisha vyuo vinavyotoa kozi za usingizi na ganzi kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada ili kukabiliana na upungufu wa wataalamu.


“Serikali pia itaendelea kuandaa na kusimamia miongozo ya utoaji wa huduma za dawa za usingizi na ganzi salama katika ngazi zote za vituo vya afya,” amesema Dkt. Samizi.


Ameongeza kuwa Serikali imeongeza bajeti ya sekta ya afya ili kuimarisha utoaji wa huduma na kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali muhimu, huku ikiendelea kutafuta vyanzo vya mapato ili kuendeleza sekta hiyo.


Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amesema Serikali imesikia changamoto zinazowakabili wataalamu hao na itaendelea kushirikiana nao kupitia vyombo vyao ili kuboresha mazingira ya kazi na utoaji wa huduma huku akiwataka wataalamu hao kuendelea kushirikiana na Serikali katika juhudi za kuokoa maisha ya wananchi kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma.



















No comments