DAR YATENGA BILIONI 1.9 KUPANDA MITI MILIONI 7.5 KULINDA MAZINGIRA

Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam imetenga shilingi bilioni 1.9 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya zoezi la upandaji miti takribani milioni 7.5, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda mazingira na kukuza uchumi endelevu kupitia sekta ya misitu.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya upandaji miti kimkoa yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Juhudi, Gongolamboto, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema kuwa halmashauri zote zimeelekezwa kuhakikisha zinahamasisha upandaji miti kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuanza kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kuanzia ngazi za awali shuleni, ili kujenga uelewa wa kudumu kwa vijana kuhusu umuhimu wa miti na mazingira kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Nurdin Bilal, ameeleza kuwa jiji hilo litaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kuhakikisha lengo la upandaji miti linafikiwa na mazingira yanabaki salama.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji, Elihuruma Mabelya, ameongeza kuwa juhudi za utunzaji wa mazingira zinaendelea kuimarishwa kwa kushirikiana na wadau wa mazingira, huku akitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo.

Hatua hiyo inaonekana kuwa chachu muhimu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, huku ikilenga kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji lenye mazingira rafiki na endelevu kwa vizazi vijavyo.

No comments