MKOA WA KAGERA WAELEKEZA TASAC NA NIC KUTOA ELIMU KUHUSU BIMA NA USALAMA WA USAFIRI MAJINI

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera imezielekeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) na Shirika la Bima la Taifa (NIC) kuimarisha utoaji wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima pamoja na masuala ya usafiri salama majini ili kupunguza ajali na hasara zinazoweza kuepukika.

Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Bw. Isaya Tendega, wakati akizungumza na maafisa kutoka TASAC na NIC waliotembelea Ofisi ya Mkuu Mkoa Kagera, leo tarehe 9 Aprili, 2026.

Bw. Tendega amesema kuwa wananchi wengi wanaotumia usafiri wa majini, hususan katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Victoria, bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa kuwa na bima pamoja na kuzingatia taratibu za usalama wanapotumia vyombo vya usafiri majini. 

“Utoaji wa elimu hiyo utasaidia kuongeza uelewa kwa wamiliki wa vyombo, waendeshaji na abiria, hivyo kuchangia kupunguza ajali pamoja na kulinda maisha na mali za wananchi,” amesema Bw. Tendega.

Kwa upande wake, Afisa Bima Mkoa wa Kagera, Bw. Alfred Bwojo, ameeleza kuwa elimu ya bima ni muhimu katika kuwasaidia wananchi kuelewa namna ya kujikinga na athari za kifedha zitokanazo na ajali au majanga na hatua za kuchukua ili kufidia majanga yanapotokea.

Aidha, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mkoa wa Kagera, Nahodha Mzee Mvihanga, ametoa rai kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri majini kuhakikisha wanazingatia viwango vya usalama, ukaguzi na matengenezo ya mara kwa mara ili kuzuia ajali na kuhakikisha usafiri wa majini unakuwa salama kwa watumiaji wote.

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano kwa Umma wa TASAC, Bw. Saidi Mkabakuli amesema kuwa TASAC itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha elimu inawafikia wananchi kwa ufanisi na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya usafiri majini.

No comments