MSD YAPONGEZWA UPATIKANAJI DAWA, HUDUMA ZA AFYA MANYONI ZAIMARIKA



Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Dk. Bwire Robert, ameipongeza Bohari ya Dawa (MSD) kwa kufanya mapinduzi makubwa ya kiutendaji katika usambazaji wa dawa na vifaa tiba kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati nchini.


Dk. Bwire amesema maboresho yaliyofanywa na MSD yamewarahisishia watoa huduma za afya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, huku yakipunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko ya wananchi kuhusu upatikanaji wa huduma.


Akizungumza leo wilayani Manyoni mkoani Singida wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea Hospitali ya Wilaya ya Manyoni kujionea huduma zinazotolewa kupitia vifaa tiba vinavyosambazwa na MSD, Dk. Bwire alieleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali yamerahisisha utoaji wa oda za dawa hadi ngazi ya kijiji na kuhakikisha zinapatikana kwa wakati.


Ameongeza kuwa uwekezaji wa Serikali katika vifaa tiba, dawa na rasilimali watu umeleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma za afya katika hospitali za wilaya. Ametolea mfano uwepo wa chumba maalum cha kuwahudumia watoto njiti, ambapo vifaa vilivyotolewa na MSD vimechangia kupunguza vifo vya watoto hao kwa takribani asilimia 90.


Dk. Bwire pia alitaja baadhi ya vifaa vilivyowezeshwa na MSD katika hospitali hiyo kuwa ni pamoja na vifaa vya kisasa vya maabara, mashine za kisasa za ultrasound, vifaa vya upasuaji pamoja na mashine za usingizi (anesthesia).


Kwa upande wake, Meneja wa MSD Kanda ya Dodoma, Mwanashehe Jumaa, amesema taasisi hiyo inahudumia zaidi ya vituo 400 vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Singida. Ameongeza kuwa katika Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Singida, Dodoma pamoja na Wilaya ya Kiteto, MSD inahudumia jumla ya vituo zaidi ya 840, huku akiahidi kuendelea kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati.









No comments