SERIKALI YAWEKA MIKAKATI KUIMARISHA SEKTA YA SHERIA KUFANIKISHA DIRA 2050.


WAZIRI wa Katiba na Sheria, Juma Homera, amesema serikali imejipanga kuimarisha sekta ya sheria ili iweze kuchangia kikamilifu kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo 2050 ya Tanzania, kwa kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utawala bora, uwajibikaji na utoaji wa huduma za kisheria nchini.


Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Homera amesema serikali itaendelea kuimarisha taasisi za utawala bora kwa kujenga uwezo wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utendaji wa taasisi za umma.


Ameeleza kuwa katika kuhakikisha sekta ya sheria inakuwa na wataalam wa kutosha na wenye ubobezi, wizara imepanga kuimarisha mafunzo na utaalam kwa kuendeleza wataalam katika maeneo mbalimbali ya sheria pamoja na kuanzisha kituo cha umahiri kitakachosaidia kukuza taaluma hiyo nchini.


Aidha, amesema serikali itaimarisha usimamizi wa mali za wadhamini kupitia ofisi ya Public Trustee kwa kuboresha huduma za mirathi na ufilisi ili kulinda mali za wanufaika na kuhakikisha haki inatendeka kwa uwazi na usawa.


Katika hatua nyingine, Homera amebainisha kuwa wizara itaimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini kwa kuanzisha mfumo wa kitaifa wa kupima utendaji katika sekta ya sheria, hatua itakayosaidia kuongeza ufanisi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi mbalimbali.


Pamoja na hayo, Homera amesisitiza kuwa serikali itaweka mifumo madhubuti ya kuimarisha nidhamu na uwajibikaji katika taasisi za umma ndani ya sekta ya sheria, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka ili kulinda rasilimali za umma na kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi za serikali.

No comments