UCSAF KUKAMILISHA UJENZI WA MINARA YA MAWASILIANO KATIKA KATA 567.


SERIKALI imeendelea kuimarisha sekta ya mawasiliano na teknolojia nchini kupitia mipango kabambe ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote na Tume ya TEHAMA, inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kidijitali na kuchochea uchumi wa kisasa.


Katika mwaka wa fedha 2026/2027, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umepanga kukamilisha ujenzi wa minara ya mawasiliano katika kata 567 zenye changamoto ya huduma za simu na intaneti, hatua itakayopanua mawasiliano hasa maeneo ya vijijini.


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Angellah Kairuki,amesema hayo April 30,2026,Bungeni Jijini Dodoma,wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027.


Amesema katika kuongeza matumizi ya intaneti, Mfuko unapanga kuunganisha huduma ya Wi-Fi katika maeneo 100 ya umma na kuboresha vituo sita vya kubadilishana intaneti (IXPs) katika miji ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Arusha na Zanzibar.


Aidha, huduma za mkongo wa taifa (fiber) zitasambazwa katika halmashauri 10 huku vituo vya TEHAMA vikikarabatiwa Unguja na Pemba. Katika sekta ya elimu, maabara za TEHAMA zitaanzishwa katika shule 250 za umma, vifaa maalum kutolewa kwa shule 10 zenye wanafunzi wenye mahitaji maalumu, na walimu 700 pamoja na wanafunzi wa kike 250 kupatiwa mafunzo ya TEHAMA.


Mfuko pia unatarajia kuanzisha redio za jamii katika wilaya tano pamoja na kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa huduma za afya kwa njia ya mtandao (telemedicine), hatua inayotarajiwa kuboresha huduma za afya hasa maeneo ya mbali.

No comments