Wanachama wa TALGWU TAMISEMI waaswa Kuwachagua Viongozi Waadilifu


Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bi. Namsifu Maduhu, amewataka wafanyakazi kuchagua viongozi waadilifu, wenye weledi na wanaojali maslahi ya wanachama, ili kuimarisha ufanisi wa chama chao mahali pa kazi.


Akifungua kikao cha uchaguzi wa viongozi wa TALGWU tawi la OWM-TAMISEMI leo Aprili 24, 2026 jijini Dodoma, Bi. Maduhu alisisitiza umuhimu wa kuchagua viongozi wenye uelewa mpana wa masuala ya kazi na uwezo wa kusimamia haki za wanachama kwa uadilifu.


Alieleza kuwa Viongozi bora ni wale watakaoweza kusimamia na kutatua changamoto za wafanyakazi, zikiwemo migogoro ya kikazi, huku akihimiza wafanyakazi kudumisha umoja na kushiriki kikamilifu katika vikao ili kuimarisha sauti yao ya pamoja.


“Chagueni viongozi wenye weledi na uelewa, watakaotufikisha mahali pazuri. Tuna migogoro mingi kazini, hivyo umoja wenu na ushiriki wenu katika vikao ni msingi wa kuwapa nguvu viongozi mtakaowachagua,” alisisitiza Bi. Maduhu.


Aidha, alibainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI imeingia makubaliano ya kuundwa Baraza la Wafanyakazi kwa kushirikiana na TALGWU na TUGHE, hatua itakayosaidia kuweka Mwongozo wa pamoja katika kushughulikia masuala ya wafanyakazi kwa ufanisi zaidi.


Kwa upande mwingine, Katibu wa TALGWU Mkoa wa Wizara na Taasisi, Happiness Makombe, aliwapongeza Viongozi waliomaliza muda wao kwa kuimarisha ushirikiano na kutatua changamoto za wafanyakazi. 


Naye Mwenyekiti aliyerejea madarakani, Bw. Amiri Mhando wa tawi la OWM-TAMISEMI, ameahidi kuendeleza mshikamano, kulinda ajira na ujira wa wanachama kwa kuzingatia sheria na miongozo, huku chama hicho kikiendelea kushirikiana na mashirika mbalimbali ikiwemo TUCTA, PSI na AMALGUN.


Viongozi waliochaguliwa ni pamoja Amiri Mhando – Mwenyekiti, Marco Ngajua - Katibu wa Tawi, Edna Mwaipopo - Mwenyekiti wa Wafanyakazi wanawake, Julieth Nyenza- Katibu wa Wafanyakazi wanawake na wajumbe ambao Tully mwamjengwa, Ainekishe John na James Mapunda.

No comments