ABIRIA MILIONI 2.51 WAMESAFIRI KWA SGR KUANZIA JULAI 2025 HADI MACHI 2026.
BUNGE limeelezwa kuwa usafirishaji kupitia reli ya kisasa ya SGR umezidi kuimarika ambapo katika kipindi cha Julai, 2025 hadi Machi, 2026 jumla ya abiria milioni 2.51 walisafirishwa ikilinganishwa na abiria millioni 2.05 waliosafirishwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 22.40.
Aidha,katika kipindi cha kuanzia Julai, 2025 hadi kufikia mwezi Machi 2026, TRC ilisafirisha jumla ya tani 102,452 za mizigo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuanza usafirishaji wa mizigo kupitia reli ya SGR.
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa,amesema hayo Mei 13,2026,Bungeni Jijini Dodoma,wakati akiwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa fedha wa 2026/2027.
Amesema katika hatua za kuunganisha miundombinu ya reli ya SGR na MGR, Serikali imeendelea na uunganishaji wa reli hizo katika eneo la Ruvu ili kuwezesha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari za Dar es Salaam na Tanga, ambapo utekelezaji wake umefika asilimia 85.
Aidha,amesema ujenzi wa kuunganisha reli za MGR na SGR unaendelea katika eneo la Bahi kwa lengo la kuwezesha uhamishaji wa mizigo kati ya reli hizo mbili na unaendelea vizuri.
pamoja na mafanikio hayo Profesa Mbarawa amesema serikali inaendelea kuboresha Reli ya MGR kwa kubadilisha reli nyepesi na kuweka nzito, pamoja na kuongeza uwezo wa madaraja.

Post a Comment