CCM ZANZIBAR YAJIPANGA KUJIIMARISHA KIUCHUMI KWA KUANZISHA MIRADI
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema wameona ipo haja ya kukiimarisha chama kiuchumi kupitia uanzishaji wa miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo kwa manufaa ya chama pamoja na wananchi kwa ujumla.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo Mei 13, 2026 katika muendelezo wa ziara yake ya kukutana na viongozi pamoja na wanachama wa CCM Kisiwani Pemba, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Tawi la Ng’ombeni Jimbo la Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema kuwa chama cha siasa ni lazima kiwe na uchumi imara, rasilimali pamoja na fedha za kutosha ili kiweze kukidhi mahitaji mbalimbali ndani ya chama pamoja na kuimarisha miundombinu yake ikiwemo ujenzi na uimarishaji wa matawi ya CCM.
Aidha, Dk. Mwinyi amesema kuwa katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025 Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo kupitia sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa skuli za ghorofa, hospitali za kisasa, huduma za maji safi na salama, michezo, ujenzi wa bandari pamoja na miundombinu ya barabara nchini.
Katika hatua nyingine, Dk. Mwinyi amesema kuwa katika kipindi kijacho wataendelea kufanya makubwa zaidi katika kuwaletea wananchi maendeleo, huku akiwataka viongozi wa CCM kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha ahadi zote zilizotolewa zinatimia na kutekelezwa kwa vitendo kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.




Post a Comment