DKT. MAGEMBE AHIMIZA WANANCHI KUFANYA MAZOEZI KULINDA AFYA ZAO




Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt.Grace Magembe, amewataka Watanzania kuchukua hatua madhubuti za kubadili mtindo wa maisha ili kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, akisisitiza kuwa mabadiliko hayo yanaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa magonjwa hayo nchini.

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya “Jua Namba Zako” uliofanyika jijini Mwanza leo Mei 4, 2026, Dkt. Magembe amesema kuwa, takwimu za kimataifa zinaonesha ongezeko kubwa la wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza, kutoka watu milioni moja mwaka 2021 hadi kufikia  watu milioni 6.5 kwa sasa. 

Aidha, ameeleza kuwa magonjwa kama shinikizo la juu la damu na kiharusi yanaathiri zaidi watu wenye umri kati ya miaka 30 hadi 45, ambao ndiyo nguvu kazi kuu ya Taifa na kuonya kuwa, kuendelea kwa hali hiyo kunaweza kudhoofisha uchumi wa familia na taifa kwa ujumla, kwani gharama za matibabu ni kubwa na mara nyingi Wananchi wengi hawawezi kumudu

"Gharama za huduma za kuchuja damu, zinakadiriwa kuwa kati ya shilingi 150,000 hadi 300,000 kwa huduma moja, jambo linaloweka mzigo mkubwa kwa familia nyingi, hivyo nasisitiza kuwa kinga ni bora kuliko tiba, na kwamba njia rahisi na yenye ufanisi zaidi ni kubadili mtindo wa maisha" amesema Dkt. Magembe.

Dkt. Magembe amesisitiza wananchi kupunguza matumizi ya chumvi na sukari kupita kiasi, kufanya mazoezi mara kwa mara ikiwemo kutembea angalau hatua 10,000 kwa siku, kuepuka matumizi ya pombe na sigara, pamoja na kupunguza matumizi ya mafuta mengi katika vyakula.

Dkt. Magembe  amesema siyo lazima mtu aende katika vituo vya mazoezi ili kuwa na afya njema, bali nidhamu ya maisha ya kila siku ndiyo msingi mkuu wa kujikinga na magonjwa haya.

"Kampeni ya “Jua Namba Zako” inalenga kuwahamasisha wananchi kufahamu hali ya afya zao kwa kupima viashiria muhimu kama shinikizo la damu, kiwango cha sukari na mapigo ya moyo, ili waweze kuchukua hatua stahiki mapema.

Daktari Magembe amesisitiza kuwa mafanikio ya mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza yanategemea ushirikiano wa kila mmoja, akihimiza jamii kuchukua jukumu la kulinda afya zao kwa kufanya maamuzi sahihi ya kila siku.


No comments