KUNENGE AKUTANA NA WATENDAJI KATA 134 PWANI



MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewaagiza watendaji wa kata mkoani humo kuchochea na kuwa chachu ya maendeleo kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato pamoja na kutatua kero za wananchi . 


Kunenge ametoa maagizo na maelekezo mbalimbali Mei 25,2026 wakati akizungumza na watendaji wa kata 134 kati ya 136 zilizopo mkoani humo ambapo amewataka kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili mkoa kuongeza mapato zaidi ifikapo Juni 2026.


Ameeleza Mkoa huo umeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato baada ya kuongezeka kutoka asilimia 87.9 mwezi Juni 2025 hadi asilimia 106 mwezi Machi 2026.


Aidha, ametoa rai kwa watendaji hao kuepuka kuingilia mihimili mingine, ikiwemo Mahakama na Mabaraza ya Ardhi, vinavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.


Hata hivyo Mkuu huyo wa mkoa amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa kuzingatia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050, ikiwemo kuongeza pato la Taifa, pato la mtu mmoja mmoja, kuzalisha ajira, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kukuza uwekezaji na viwanda.






No comments