RIDHIWANI KIKWETE AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA MKUTANO WA BAJETI WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, Jana Mei 22, 2026 jijini Arusha ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo ni hatua muhimu ya maandalizi ya Bajeti ya Jumuiya hiyo kabla ya kuwasilishwa katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa kabla ya Juni 30, 2026.
Katika mkutano huo, Mhe. Ridhiwani Kikwete aliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Cde. James Millya; Naibu Waziri wa Fedha Cde. Mshamu Ali Munde; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu anayesimamia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Said Shaibu Mussa; pamoja na maafisa wengine waandamizi wa Serikali.
Aidha, katika Mkutano huo wamejadili mipango ya kibajeti ya Taasisi mbalimbali ikiwemo Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, Bunge la Afrika Mashariki, Taasisi ya Bonde la Ziwa Victoria na Nyenginezo. Pia, Mkutano huo umepokea hati idhini za kisheria za utambuzi rasmi wa Jamhuri ya Sudan Kusini kuwa Mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya Bunge la nchi hiyo kupitisha sheria ya kutambua uanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.




Post a Comment