SERIKALI YAENDELEA KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA EBOLA
Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa Ebola kwa kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa huo hatari.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Samuel Laizer wakati wa mkutano ya ujirani mwema kati ya Tanzania na Uganda iliyolenga kujadili masuala ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza katika maeneo ya mipakani pamoja na mipango ya dharura za afya kwa maeneo ya mipaka ya Mutukula na Kabanga, Mkoani Kagera.
Dkt. Laizer amesema juhudi hizo zinafanyika kupitia majukwaa mbalimbali ya kijamii pamoja na ushirikishwaji wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wamepewa jukumu la kuwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu, hususan maeneo ya mipakani.
Ameeleza kuwa tayari watalaam hao wameanza kutoa elimu katika maeneo ya mipaka isiyo rasmi kati ya Tanzania na nchi jirani, huku magari yenye vifaa vya matangazo yakipita katika maeneo mbalimbali kutoa ujumbe wa tahadhari na mbinu za kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Ebola.
Ameongeza kuwa hatua hizo zinalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu dalili za ugonjwa huo, umuhimu wa kutoa taarifa mapema pamoja na kuhimiza wananchi kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kuzuia hatari ya maambukizi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Mazingira na Usafi, Dkt. Amour Selemani amepongeza ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Uganda katika kuimarisha ufuatiliaji wa afya mipakani, utoaji wa elimu kwa jamii pamoja na hatua za haraka za tahadhari zinazochukuliwa ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii na kuenea ndani ya nchi.
Naye Mkuu wa Huduma za Afya Mipakani kutoka Wizara ya Afya, Remigius Kakuru, amesema kuwa kuimarisha elimu kuhusu ugonjwa wa Ebola katika maeneo ya mipakani ni hatua muhimu katika kuzuia kuingia na kuenea kwa ugonjwa huo nchini kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu kutoka sehemu mbalimbali.
Ameongeza kuwa utoaji wa elimu sahihi kuhusu dalili za ugonjwa, njia za maambukizi na hatua za kujikinga utaongeza uelewa na tahadhari kwa wananchi na wasafiri, huku ukiimarisha uwezo wa jamii kuchukua hatua za mapema za kinga na udhibiti
Post a Comment