SERIKALI YATOA SHILINGI BILIONI 21 KUREKEBISHA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIWA NA MVUA

Serikali imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni 21  kwa halmashauri mbalimbali nchini ili kurekebisha miundombinu ya barabara iliyoathiriwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali, hatua inayolenga kurejesha huduma za usafiri na shughuli za kijamii kwa wananchi. 

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Dkt. Festo Dugange kwa Niaba ya Waziri wa Nchi, OWM-TAMISEMI, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Bagamoyo, Mhe. Subira Khamis Mgalu, leo Mei 06, 2026, Bungeni jijini Dodoma, aliyetaka kufahamu ni ini Serikali itaanza utekelezaji wa Mradi wa TACTIC katika Jimbo la Bagamoyo baada ya usanifu kukamilika.

Amesema kuwa maeneo mengi yameathirika kutokana na mvua hizo, hali iliyosababisha baadhi ya barabara kutopitika, hivyo Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeelekeza mameneja wa wilaya na mikoa kuchukua hatua za haraka kurekebisha miundombinu hiyo kwa kiwango kinachowezekana. 

Akijibu hoja za Mbunge wa Bagamoyo, Mhe. Subira Khamis Mgalu, kuhusu ubovu wa barabara na athari zake kwa wananchi na wawekezaji, Dkt. Dugange amesema Serikali inaendelea pia na mipango ya muda mrefu kupitia miradi ya maendeleo ikiwemo ule wa TACTIC unaohusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami pamoja na stendi kuu ya mabasi ya Bagamoyo. 

“Tayari maelekezo yametolewa kwa wataalam kuhakikisha maeneo yaliyoharibika yanapatiwa ufumbuzi wa muda ili kupunguza adha kwa wananchi wakati wakisubiri utekelezaji wa kudumu wa miradi hiyo,” amesema Dkt. Dugange.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu maeneo yaliyoathirika zaidi ili kuhakikisha huduma za usafiri zinarejea katika hali ya kawaida haraka iwezekanavyo, huku ikiweka mikakati madhubuti ya kudhibiti athari za majanga ya mvua kwa miundombinu ya barabara nchini.

No comments