TAKUKURU IRINGA YASAIDIA IRINGA KUKUSANYA MILIONI 44.



Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa-TAKUKURU, mkoani Iringa imesaidia kupandisha makusanyo ya ushuru wa vibali vya usafirishaji wa mifugo kwenye minada ya kimande na Nyang'oro hadi kufikia zaidi ya shilingi Millioni-44.

Hayo yamebainishwa na mkuu wa TAKUKURU Mkoa, Victor Swella, wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi katika kipindi cha Januari-Machi 2026 mbele ya waandishi wa Habari, amesema, baada ya kufanya uchambuzi wa mfumo wa makusanyo ya mapato katika minada ya mifugo, ilibaini mianya ya rushwa na mapungufu yaliyopo katika ukusanyaji wa ushuru wa vibali vya usafirishaji wa mifugo na kuwezesha Halmashauri ya wilaya ya Iringa kufikia kiasi hicho.


Kupanda kwa mapato hayo kumetokana na uchambuzi wa mfumo wa taratibu za ulipaji wa ushuru,usimamizi na ukusanyaji mapato uliofanywa na Takukuru na kubaini mianya ya rushwa ikiwemo udanganyifu, kuwepo kwa utoroshaji wa mifugo kutokana na eneo la mnada kutokuwa na uzio.

Amesema, katika kipindi tajwa TAKUKURU ilifuatilia matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi 28 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni- 13.

Ili kuleta ufanisi, TAKUKURU ilishauri kuandaa Mafunzo kwa mafundi ili wajue  namna ya  kutumia mfumo  wa Nest na Mafunzo yalifanyika katika Halmashauri zote kwa kishirikiana na PPRA.

No comments