TANZANIA NA ALGERIA ZAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIHISTORIA KATIKA ULINZI NA USALAMA



Mahusiano kati ya Tanzania na Algeria ni sehemu ya urithi mkubwa wa mshikamano wa bara la Afrika uliojengwa katika kipindi cha harakati za ukombozi wa Afrika na mapambano dhidi ya ukoloni. 


Tangu enzi za viongozi waasisi kama Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kanali Mohamed Ben Brahim Boukhrouba aliyefahamika pia kama Houari Boumédiène, nchi hizi mbili zimekuwa zikishirikiana katika kulinda uhuru, mshikamano wa Afrika na kujenga misingi ya usalama wa kikanda.


Kikao kati ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho, na ujumbe wa Jeshi la Algeria ulioongozwa na Brigedia Jenerali Abbas Ibrahim katika ofisi ndogo za Wizara Upanga, Jijini Dar - Es - Salaam kinaonesha wazi kuwa mahusiano hayo ya kihistoria sasa yanaingia katika hatua mpya ya ushirikiano wa kimkakati wa kisasa. 


Katika dunia ya sasa yenye changamoto za ugaidi, uhalifu wa kimataifa, migogoro ya kikanda na ushindani wa kiusalama, mataifa ya Afrika yanazidi kuona umuhimu wa kushirikiana katika mafunzo ya kijeshi, kubadilishana uzoefu wa kiintelijensia na kuimarisha uwezo wa majeshi yao.


Algeria ni moja ya mataifa yenye uzoefu mkubwa wa kijeshi na usalama barani Afrika, hususan katika mapambano dhidi ya ugaidi na kulinda mipaka yake. Kwa upande mwingine, Tanzania imeendelea kujijengea heshima kimataifa kama taifa lenye amani, utulivu na mchango mkubwa katika operesheni za kulinda amani Afrika. Ushirikiano kati ya majeshi ya nchi hizi mbili unaweza kusaidia kuongeza uwezo wa kitaalamu, teknolojia za kiulinzi na ujenzi wa majeshi yenye weledi zaidi. 


Brigedia Jenerali Abbas aliwasilisha pongezi zilizotolewa na Rais wa Algeria, Mheshimiwa Abdelmadjid Tebboune, kwa uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuhusu kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini. Pongezi hizo zinaonesha namna ambavyo Tanzania inaendelea kuaminiwa kimataifa kama nguzo ya utulivu katika ukanda wa Afrika Mashariki.


Kwa mtazamo wa kidiplomasia, kikao hiki si tu mazungumzo ya kijeshi, bali pia ni ishara ya kuimarika kwa diplomasia ya ulinzi kati ya mataifa ya Afrika yenye historia ya urafiki na mshikamano. Ushirikiano huu unaweza kufungua milango ya mafunzo, uwekezaji katika sekta za ulinzi, teknolojia za kijeshi na ushirikiano mpana wa kiusalama kwa manufaa ya mataifa yote mawili na bara la Afrika kwa ujumla.



No comments