TANZANIA NA UTURUKI ZASAINI MKATABA WA KUONDOA UTOZAJI KODI MARA MBILI (DTA)



Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Uturuki, zimesaini Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi Mara Mbili (Double Taxation Agreement - DTA) ili kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuongeza wigo wa uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.


Mkataba huo umesainiwa na Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Balozi wa Jamhuri ya Uturuki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Bekir Gezer,  Kwa niaba ya Jamhuri ya Uturuki tarehe 04 Mei, 2026 jijini Dar es Salaam


Mhe. Balozi Omar amesema Mkataba huo unasaidiana na Mkataba wa Kulinda Vitega Uchumi kwa mataifa yote mawili uliosainiwa mwaka 2011 ili kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa kuondoa kikwazo cha mlipakodi mmoja kutozwa kodi katika nchi zote mbili kwa kipato kilekile.


Mhe. Omar amesema utekelezaji wa mkataba huo utaimarisha mtiririko wa teknolojia, mitambo ya kisasa na ujuzi kutoka Uturuki, sambamba na kupanua masoko ya bidhaa za Tanzania ikiwemo mazao ya kilimo, ufugaji, uvuvi na madini katika soko la Uturuki. 


Waziri Omar amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuimarisha diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa kikanda kupitia juhudi zake za kuvutia uwekezaji na kuimarisha mahusiano ya kimataifa, ambazo zimechangia kukuza maendeleo ya taifa.


Ameongeza kuwa utekelezaji wa mkataba huu utachochea kasi ya uwekezaji, kupunguza gharama za biashara, na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Uturuki, ukilenga kufikia thamani ya biashara ya Dola Bilioni Moja za Marekani.

 

Akizungumza katika hafla iliyofanyika sambamba na Mkutano wa kwanza wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Uturuki, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, aliishukuru Serikali ya Uturuki kwa kuimarisha uhusiano wa kimkakati na Tanzania, kwani umesaidia kuleta maendeleo ya wananchi wa pande zote mbili, hususan katika sekta za biashara, uwekezaji, elimu, afya, ulinzi, nishati, kilimo na utalii.

No comments