WANANCHI MILIONI 15 HADI 20 KUNUFAIKA NA KAMERA ZA FUNDUS INAYOFANYA UCHUNGUZI WA MAGONJWA YA KISUKARI
Kaimu Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyoambukizwa kutoka Wizara ya Afya, Edith Bakari amesema uwepo teknolojia ya Kamera za Fundus (Portable Fundus Camera) zinazotumika kufanya uchunguzi wa mapema wa athari za ugonjwa wa kisukari kwenye pazia la jicho (diabetic retinopathy) unatararajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi kati ya Milioni 15 hadi 20 wa mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na maeneo jirani inayozunguka nikoa hiyo
Akizungumza wakati wa mafunzo ya matumizi ya kamera hizo yaliyofanyika katika hospitali ya Benjamini Mkapa Bi. Bakari amesema kuwa, kupitia teknolojia hiyo wagonjwa wataweza kugunduliwa mapema kabla ya kufika hatua za hatari hivyo, kuwezesha kuanza matibabu mapema na kupunguza au kuzuia kabisa ulemavu wa kutokuona unaosababishwa na ugonjwa wa kisukari.
“Vifaa hivi vinatarajiwa kutumika kikamilifu katika kliniki za wagonjwa wa kisukari zilizopo hospitali zetu na katika huduma za mkoba, hii itasaidia kuwafikia wananchi wengi ambao hawafiki kwa urahisi katika vituo vya kutolea huduma za afya” amesema Bi. Edith
Aidha ameishukuru London School of Hygiene and Tropical Medicine (LSHTM) ambayo imekuwa ikishirikiana na kwa karibu na Wizara ya Afya ili kutekeleza afua mbalimbali za uboreshaji wa huduma za macho.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Huduma za Macho kutoka Wizara ya Afya Dkt. Eunice Headcraph amesema kuwa baada ya mafunzo haya kwa wataalam kutoka kwenye hospitali zilizopokea kamera hizo (Benjamini Mkapa, Muhimbili-Mloganzila na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya), kila kituo kinatarajiwa kuanza utekelezaji wa huduma hii muhimu.
Amefafanua kuwa ni muhimu kwa wataalam hao kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kikamilifu, huku utekelezaji ukienda sambamba na kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa kila mwezi zikionesha idadi ya wagonjwa waliohudumiwa, waliokutwa na changamoto, waliopatiwa matibabu na aina ya matibabu yaliyotolewa.









Post a Comment