TANZANIA YAJIPAMBANUA KUWA KINARA WA UONGOZI WA WANAWAKE AFRIKA



TANZANIA imeendelea kujijengea hadhi ya kuwa kinara wa ushiriki wa wanawake katika uongozi baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wabunge Wanawake kutoka nchi 12 za Ukanda wa Maziwa Makuu utakaofanyika Novemba 2 hadi 5 mwaka huu jijini Dar es Salaam.


Mkutano huo wa Jukwaa la Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR), linalojihusisha na masuala ya amani, usalama, demokrasia na maendeleo, unaotarajiwa kuwakutanisha wabunge wanawake kujadili mchango wao katika kujenga ukanda salama na wenye maendeleo.


Akizungumza baada ya kusainiwa kwa makubaliano kati ya Bunge la Tanzania na Sekretarieti ya ICGLR, Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema Tanzania imepewa heshima hiyo kutokana na rekodi yake katika kutetea haki za wanawake na kukuza ushiriki wao katika uongozi.


Amesema Tanzania ipo tayari kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali na kuhakikisha mkutano huo wa kihistoria unafanyika kwa mafanikio makubwa.


Katibu wa Bunge, Baraka Leonard amesema maandalizi yote muhimu yakiwemo huduma za malazi, chakula na usafiri yatazingatiwa ili kuhakikisha wageni wanapata huduma bora wakati wote wa mkutano.


Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya ICGLR, Balozi Dkt Deo Mwalongo amesema Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji kutokana na mchango wake mkubwa katika masuala ya jinsia, amani na usalama ndani ya ukanda huo.


Amesema pia historia ya kuanzishwa kwa sekretarieti hiyo ina mizizi Tanzania, ambapo wazo la kuanzishwa kwake lilizaliwa mwaka 2004 wakati wa uongozi wa hayati Benjamin Mkapa.


Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake bungeni, ikiwa na asilimia 38 ya wabunge wanawake.


Mwakilishi wa Tanzania katika jukwaa hilo, John Chewelesa amesema mkutano huo unakuja wakati ukanda wa Maziwa Makuu ukiendelea kukabiliwa na changamoto za migogoro katika mataifa kama DRC, Sudan Kusini na Sudan.


Amesema wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa wa migogoro hiyo, hivyo mkutano huo utatoa nafasi ya kujadili namna ya kujenga ukanda wenye amani na usalama wa kudumu.


Naye Mbunge wa Viti Maalum, Sylivia Sigula amesema uwepo wa Rais mwanamke nchini Tanzania unatoa nafasi kubwa ya kuendeleza mjadala kuhusu amani, malezi na maendeleo ya jamii kupitia uongozi wa wanawake.


Jukwaa la ICGLR lina wanachama 12 ambao ni Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Congo, DRC, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Uganda, Zambia na Tanzania, huku makao makuu ya sekretarieti yake yakiwa Kinshasa, DRC.








No comments