TMDA NA WADAU WASHIRIKI MJADALA WA JOPO LA MEZA DUARA KUJADILI TATHIMINI YA MAFANIKIO NA UBUNIFU
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba
(TMDA) pamoja na wadau mbalimbali wameshiriki mjadala wa jopo la meza ya duara
uliofanyika katika siku ya mwisho ya utekelezaji wa Mradi wa BREEDIME, kwa lengo
la kutathmini mafanikio, ubunifu na uendelevu wa taasisi uliopatikana kupitia
mradi huo.
Mjadala huo uliwakutanisha
washirika wa muungano wa mradi pamoja na wadau muhimu kutoka taasisi za afya,
udhibiti wa dawa na utafiti, ambapo walijadili athari za mradi katika
kuimarisha mifumo ya udhibiti na utayari wa kukabiliana na dharura za afya ya
umma.
Katika kikao hicho, washiriki
walifanya mijadala ya kina kuhusu namna ya kusambaza matokeo ya mradi kupitia
machapisho mbalimbali ya kitaalamu, mikakati ya kuhakikisha uendelevu wa
matokeo yaliyopatikana pamoja na mwelekeo wa baadaye wa ushirikiano kati ya
taasisi husika.
Washiriki walieleza kuwa mradi wa
BREEDIME umeonesha ufanisi mkubwa katika kufanikisha malengo na matokeo
yaliyopangwa, huku ukiendelea kuwa na mchango muhimu katika kukidhi mahitaji ya
mifumo ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba.
Aidha, ilielezwa kuwa matokeo ya
awali ya mradi yanaashiria mafanikio makubwa katika kuimarisha uwezo wa taasisi
mbalimbali, ingawa uendelevu wake utategemea namna taasisi zitakavyoendelea
kuupa kipaumbele na kutoa ushirikiano wa muda mrefu.
Kwa ujumla, wadau walikubaliana
kuwa Mradi wa BREEDIME umeweka msingi imara wa kuboresha mifumo ya udhibiti na
kuimarisha utayari wa kukabiliana na dharura za afya ya umma Tanzania Bara,
Zanzibar na Rwanda.
Miongoni mwa taasisi
zilizoshiriki ni TMDA, Karolinska Institutet, Kilimanjaro Clinical Research
Institute – KCRI, Muhimbili University of Health and Allied Sciences, Zanzibar
Food and Drug Agency – ZFDA, National Institute for Medical Research, Rwanda
Food and Drugs Authority pamoja na University of St Andrews.



Post a Comment