WANUFAIKA WA MIKOPO YA ELIMU YA JUU 2026/2027 WAONGEZEKA
SERIKALI imeeleza kuendelea kuweka mkazo katika kuongeza fursa za elimu ya juu nchini kwa kupanua udahili wa wanafunzi pamoja na kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo na ufadhili wa masomo ya sayansi na teknolojia.
Katika mpango huo, Serikali itaratibu udahili wa wanafunzi 180,000 wanaotarajiwa kuomba kujiunga na programu mbalimbali za shahada ya kwanza katika vyuo vya elimu ya juu nchini.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,Mei 7,2026,Bungeni Jijini Dodoma,Waziri wa wizara hiyo Profesa Adolf Mkenda,amesema pia imepanga kuongeza idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kutoka wanafunzi 252,773 katika mwaka wa fedha 2025/2026 hadi wanafunzi 292,981 mwaka 2026/2027 ili kuwezesha vijana wengi zaidi kupata elimu ya juu.
Aidha,amesema Serikali itaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi 24,978 wa ngazi ya stashahada katika fani za sayansi na ufundi ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika maendeleo ya taifa.
Katika kuimarisha zaidi sekta ya sayansi, teknolojia na ubunifu, Serikali itaendelea kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).

Post a Comment