UWEKEZAJI WA NSSF MKULAZI WACHOCHEA AJIRA, WAPUNGUZA NAKISI YA SUKARI



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi ni mradi wa kimkakati unaotekeleza kwa vitendo maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kujenga uchumi imara, shindani na shirikishi, sambamba na kufikia Dira ya Taifa ya 2050 na kuongeza fursa za ajira.


Akizungumza, wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii ilipotembelea mradi huo mkoani Morogoro, Sangu aliipongeza kamati hiyo kwa ufuatiliaji wake, akibainisha kuwa maelekezo 11 yaliyotolewa awali tayari yameingizwa katika utekelezaji, hatua inayoimarisha uwajibikaji na ushirikiano kati ya Bunge na Serikali.


Aidha, amesema mradi huo umeanza kurekodi mafanikio kwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 2,176 katika msimu huu, huku ukitarajiwa kufikia ajira 2,315 za moja kwa moja na 9,000 zisizo za moja kwa moja kadri uzalishaji unavyopanuka, Uzalishaji wa tani 50,000 za sukari unatarajiwa kupunguza nakisi ya bidhaa hiyo nchini kwa takribani asilimia 20.


Amesisitiza kuwa uwekezaji wa mifuko ya hifadhi ya jamii, ikiwemo NSSF, unaelekezwa kwenye miradi yenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na uchumi wa taifa.


Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Mchafu Chakoma, amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali kupitia NSSF kwa kushirikiana na SHIMA katika mradi huo, akieleza kuwa umeendelea kuleta tija kwa taifa na jamii kwa ujumla.


Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya kamati, Kafiti Kafiti amebainisha kuwa matarajio ni kiwanda kuanza kupata faida katika mwaka wa fedha ujao, jambo litakaloongeza mapato ya Serikali na kulinda uwekezaji wa fedha za wanachama wa NSSF, huku kamati ikiendelea kusimamia mradi huo ili kuhakikisha unafikia malengo yaliyokusudiwa.










No comments