ZANZIBAR YAJIFUNZA KUTOKA MUHIMBILI KUANZISHA HOSPITALI YA RUFAA YA KISASA



Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) leo May 6, 2026 imepokea ujumbe maalum kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar uliowasili ili kujifunza namna ya kuanzisha hospitali ya rufaa ya kisasa visiwani Zanzibar.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi MNH, Dkt. Delilah Kimambo ameeleza kuwa Muhimbili ipo tayari kushirikiana na wadau na tasisi mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya nchini ambapo amefafanua hospitali hiyo imeendelea kuimarisha huduma zake kwa kuwekeza katika wataalam wabobezi, teknolojia ya kisasa pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya tiba na uchunguzi.


“Muhimbili itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kutoa ushauri, mafunzo na utaalamu ili kuhakikisha azma ya kuanzisha hospitali ya rufaa ya kisasa inafanikiwa na kutoa huduma bora kwa wananchi. Nia na kusudi ni kuhahakikisha kuwa kila mtanzania anapata huduma za kibobezi kwa ukaribu na bila kutumia gharama kubwa” amesema Dkt. Kimambo.


Kwa upande wake, Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum, SMZ Ndg. Mikidadi Mbarouk Mzee ameipongeza MNH jinsi ilivyojipanga katika utoaji wa huduma za kibingwa, hususan matumizi ya teknolojia ya kisasa na kubainisha kuwa uzoefu walioupata utakuwa chachu muhimu katika kufanikisha mpango wa ujenzi wa hospitali ya rufaa yenye viwango vya kisasa Zanzibar.





No comments