MTEMERE YAFUNGUKA RASMI: NDEGE YA KWANZA YATUA NA WATALII ZAIDI YA KUMI KUASHIRIA MWANZO MPYA
Ukurasa mpya umefunguliwa katika historia ya utalii nchini, kwa uwanja wa ndege wa Mtemere uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Nyerere kupokea ndege ya kwanza yenye watalii zaidi ya kumi tangu kuzinduliwa kwake februari 11, 2026 baada ya kukamilika kwa taratibu za ndani na za Kimataifa za ulinzi na kiusalama kwa abiria, ndege na uwanja.
Hatua iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na shauku kubwa kwa wadau wa usafirishaji wa Anga ndani na nje ya nchi hasa kwa watalii wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere.
Wakati akishuhudia kutua kwa ndege ya kwanza leo mei 06, 2026 tangu kukamilika kwa ujenzi huo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ephraim Mwangomo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere alisema;
“Kuanza kutumika kwa uwanja huu wa Mtemere baada kutimiza taratibu za kimataifa kunafungua ukurasa mpya wa safari za Anga, kwani umekuja kipindi sahihi ambacho tunajiandaa kwa msimu mpya wa utalii (high season).”
Aidha, Kamishna Mwangomo aliongeza kuwa uwanja huo umejengwa kwa tabaka gumu, ambapo ndege ina uwezo wa kutua kipindi chote iwe kiangazi au masika tofauti na ilivyokuwa awali ambacho wakati wa mvua ndege zilikuwa hazitui hivyo kupunguza idadi ya watalii kipindi cha masika na watalii wanapopungua na mapato pia hushuka kitu ambacho kwa sasa hakitakuwepo.
Pia, Kamishna Mwangomo alimshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha za uboreshaji wa uwanja wa ndege huo sambamba na miundombinu mingine ya malazi kwa watalii (cottages), mahali pa kupumzikia (picnic sites), mitambo pamoja na uboreshaji wa barabara.
Uwanja wa ndege wa Mtemere, ni miongoni mwa viwanja vikubwa vya ndege vilivyomo ndani ya Hifadhi za Taifa Tanzania ukiwa na sifa ya kipekee ya kuwa na mnara wa kuongozea ndege (control tower).
Sambamba na sifa hizo pia una barabara ya kurukia (runways) yenye urefu wa kilomita 1.8, barabara ya usalama (lasser) yenye urefu wa mita 300, stopway mita 60 na clearway mita 300. Runways imetengenezwa kwa tabaka gumu liitwalo “polymer” ambayo haituamishi maji na ni rafiki kwa mazingira ya hifadhini.
Akiishusha ndege ya “MyFly Aviation” kwa madaha Rubani Abdull Hakeem Othman alisema; “Hii ni mara ya kwanza katika historia yangu ya urubani kutua katika uwanja “smooth” kama huu wa Mtemere tangu nianze safari za kusafirisha watalii katika maeneo yaliyohifadhiwa kama Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba ndani na nje ya Tanzania, hii inatutia moyo marubani na inapunguza mitikisiko inayopelekea matengenezo ya mara kwa mara ya ndege zetu.”
Hata hivyo Bw. Othman aliwasihi na kuwahamasisha marubani wenzake kutumia uwanja huo kwani taratibu zote za kiusalama ziko vizuri. Hata hivyo alichagiza na kuongeza kuwa kwa sasa Mtemere ipo kwenye viwango vya kimataifa tofauti na ilikuwa awali kabla ya uwekaji wa hilo tabaka gumu (polmer) ambayo haina mitikisiko kama ilivyo kwa changarawe au lami.
Naye, Afisa Uhifadhi Mkuu Idrisa Washington Mkuu wa cha Kitengo cha Ulinzi, Usalama na Huduma za Viwanja vya Ndege - TANAPA, alisema kuwa viwanja vya ndege huanza kufanya kazi kwa kukidhi vigezo na taratibu za ndani (TCAA) na Shirika la Usimamizi wa Usafiri wa Anga Duniani (ICO).
“Hivyo, ili viwanja vya ndege vianze usafirishaji ni lazima taratibu hizo zifanyiwe kazi. Mtemere imetimiza vigezo hivyo na sasa utaendelea kupokea ndege kama kawaida katika uwanja huo,” alimalizia Mhifadhi- Washington.
Kuanza kutumika kwa Uwanja wa Mtemere leo kutaongeza fursa za uwekezaji, kuvutia watalii zaidi na kuchagiza ongezeko la mapato ya utalii nchini Tanzania

Post a Comment