ANTONIA VERNA WAPATIWA UCHUNGUZI, ELIMU YA SIKO SELI
Uchunguzi wa kinasaba pamoja na elimu kuhusu Siko Seli, imefikishwa kwa wazazi na walezi wenye watoto wanaopatiwa huduma ndani ya Kituo cha Utengamao cha Antonia Verna, Jijini Dar es Salaam.
Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Siko Seli Tanzania-SCDPCT, kwa ushirikiano na Serenox Africa, wamefika katika kituo hicho ikiwa ni mwendelezo wa kusherehekea Siku ya Siko Seli Duniani.
Tukio hilo limefanyika Juni 20, 2026 ambapo Antonia Verna Community iliandaa marathon maalum iliyoshirikisha wanajamii pamoja na kuweka fursa ya uchunguzi na elimu ya afya kwa magonjwa mbalimbali.
Afisa Habari wa SCDPCT, Veronica Mrema, akizungumza na wananchi waliofika kwenye tukio hilo, amewahimiza hasa vijana kuchukua hatua ya kufanya uchunguzi wa hali zao za vinasaba mapema, huku jumla ya watu 15 wakijitokeza kuchunguza vinasaba, ambapo matokeo yalionesha wote walikuwa na vya kawaida, AA.
Kwa nyakati tofauti, wazazi na walezi wa watoto hao, wameeleza wamefarijika mno kwa kufikishiwa huduma hiyo, wakisema baada ya kupata elimu hiyo, wameondoka na uelewa mpya kuhusu ugonjwa wa Siko Seli na kuahidi kuendelea kuelimisha wengine.

.jpeg)


Post a Comment