BALOZI OMAR AWATAKA WALIPAKODI KUENDELEA KULIPA KODI KWA HIARI



Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amewataka walipakodi nchini kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari, kwa wakati na kwa ukamilifu,  kwa kuwa mapato ya ndani ndiyo yanayowezesha Serikali kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.


Akizungumza wakati wa Hafla ya Mbio na Matembezi ya Shukrani kwa Mlipakodi, iliyofanyika jijini Dar es Salaam, kuelekea Tuzo za Rais kwa Mlipakodi Bora pamoja na Maadhimisho ya Miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA.


Balozi Omar amesema Serikali inaitegemea -TRA kukusanya takribani Shilingi trilioni 36 katika mwaka wa fedha 2026/2027, ikiwa ni sehemu ya mapato ya ndani yanayotarajiwa kufikia shilingi trilioni 46, ambayo yatachangia zaidi ya asilimia 34 ya bajeti ya Serikali.


Amesema mafanikio ya ukusanyaji wa mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026 yanaonesha ushirikiano mzuri kati ya Serikali na walipakodi, huku akieleza kuwa mwezi uliopita TRA ilivuka lengo la ukusanyaji kwa asilimia tatu na kueleza matumaini ya kufikia malengo ya mwaka mzima ifikapo Juni 30.


Aidha, Balozi Omar amebainisha kuwa maendeleo makubwa yanayoendelea kushuhudiwa nchini, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa -SGR, uboreshaji wa Reli ya TAZARA pamoja na Mradi wa Kufua Umeme wa Bwawa la Julius Nyerere, yametekelezwa kwa kiasi kikubwa kupitia mapato yanayotokana na kodi zinazolipwa na wananchi na wafanyabiashara.


Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa -TRA Yusuph Juma Mwenda, amesema ushirikiano mzuri kati ya TRA na walipakodi umeendelea kuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya ukusanyaji wa mapato nchini.








No comments