DKT. KIJAJI ASHIRIKI KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), leo Juni 5, 2026, ameshiriki Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani na kupokea Tuzo ya Heshima kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Tuzo hiyo imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia masuala ya Mazingira kupitia Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi, ikiwa na maana ya kutambua uongozi mahiri wa Rais Samia na dhamira yake ya dhati katika kuimarisha agenda ya uhifadhi wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuendeleza maendeleo endelevu nchini.
.
Heshima hiyo ni ishara ya kutambua mchango mkubwa wa Rais Samia katika kuhamasisha na kusukuma mbele ajenda za mazingira pamoja na utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Pia, imemtambua kama kinara wa matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini, hatua ambayo imeendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, akizungumza katika maadhimisho hayo,ambapo alikuwa Mgeni Rasmi akimuwakilisha Rais Samia, Maamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameutaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha kunakuwa na miche ya kutosha kwa ajili ya kuendeleza juhudi za upandaji miti na uhifadhi wa mazingira nchini, ikiwemo kuimarisha udhibiti na usimamizi wa maeneo yote yanayopandwa miti.
Vilevile, ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuendelea kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa maeneo oevu ili kuhakikisha yanaendelea kuchangia katika uhifadhi wa mazingira, bioanuwai na maendeleo endelevu ya taifa.
Aidha, Makamu wa Rais ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutunza na kuhifadhi mazingira ili kuhakikisha rasilimali za asili zinadumu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Post a Comment