VIJANA 100 WAINGIA SHINDANO LA UCHUMI CHALLENGE 2026.
Ushindani mkubwa uliohusisha maombi 7,852 kutoka mikoa yote ya Tanzania umezaa orodha ya vijana 100 bora waliofanikiwa kutinga hatua inayofuata ya Shindano la Vijana Uchumi Challenge 2026.
Akizungumza Juni 5,2026, Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Amina Sanga, amesema mwitikio wa vijana katika shindano hilo ulikuwa mkubwa, jambo linaloonesha namna vijana wanavyoendelea kujitokeza na mawazo bunifu yanayoweza kusaidia kukuza uchumi wa Taifa.
Amesema sekta ya TEHAMA na huduma za kidigitali ndiyo iliongoza kwa asilimia 30.7 ya mawazo yaliyowasilishwa, ikifuatiwa na kilimo na teknolojia za kilimo kwa asilimia 27.8, huku sekta ya viwanda na uzalishaji ikichangia asilimia 21.3 ya mawazo yote yaliyopokelewa.
Kwa mujibu wa Sanga, baada ya uchambuzi wa awali, maombi 4,121 sawa na asilimia 52.5 yalifanikiwa kutimiza vigezo vya msingi vya shindano. Kati ya hayo, mawazo 458 yalipata alama za juu na kuingia hatua ya mwisho ya tathmini kabla ya kupatikana washiriki 100 bora waliotangazwa rasmi.
Shindano hilo lenye kaulimbiu ya “Wanafikiri, Taifa Linasonga” linalenga kuibua mawazo bunifu ya vijana yatakayosaidia kukabiliana na athari za misukosuko ya kiuchumi duniani huku likiunga mkono maono ya Serikali ya Awamu ya Sita na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, washiriki 100 bora wataingia katika kambi maalum ya mafunzo ya siku nne ambapo watapatiwa mafunzo ya kitaalamu na ushauri wa kuboresha mawazo yao kabla ya kufanya mawasilisho yatakayochuja washiriki 30 bora wa nusu fainali na hatimaye 10 bora watakaoingia hatua ya fainali.


.jpeg)
Post a Comment