MARUFUKU MADUKA VIRUTUBISHO KUGEUZWA KLINIKI:BARAZA TIBA ASILI
Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala nchini limepiga marufuku tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kugeuza maduka ya virutubisho vya chakula (food supplements) kuwa kliniki za matibabu.
Onyo hilo limetolewa Juni 05, 2026 na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Prof. Nicolao Joseph Otieno, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara ya Afya mkoani Dodoma.
Prof . Otieno amesema Baraza limebaini uwepo wa wimbi kubwa la ukiukwaji wa sheria ambapo virutubisho vinavyopaswa kutumika kama nyongeza tu ya lishe vimekuwa vikitangazwa kama dawa za kutibu au kuzuia magonjwa kinyume cha usajili wake.
Hatua hiyo inalenga kukomesha udanganyifu wa kitabibu na matangazo ya kilaghai yanayopotosha umma, amefafanua kuwa baadhi ya maduka hayo yamegeuzwa kuwa kliniki bubu ambazo hufanya uchunguzi wa afya kwa kutumia vifaa visivyosajiliwa kama vile Quantum Analyzing Machines, na kutoa ushauri wa kitabibu bila kuwa na wataalamu wenye sifa zinazotambulika kisheria.
Baraza limepiga marufuku vitendo hivyo mara moja na kuagiza wafanyabiashara hao kubaki kwenye misingi ya usajili wa bidhaa zao, Ili kudhibiti soko la tiba asili na Tiba mbadala.
Katika hatua nyingine Baraza limewakumbusha wafanyabiashara kuwa, utangazaji wa dawa au huduma yoyote bila kibali ni kosa la kisheria. Kwa mujibu wa kifungu cha 15(1) cha Kanuni za Dawa Asili za mwaka 2008, mganga, chombo cha habari, au mmiliki wa mtandao wa kijamii atakayebainika kurusha matangazo hayo bila ithibati ya Baraza atatozwa faini isiyopungua shilingi milioni moja.
Baraza limesisitiza kuwa vyombo vya habari na wadau wote wa mawasiliano wanapaswa kuwa makini na kuhakikisha matangazo yoyote ya huduma za afya yanayofika mbele yao yanaambatana na kibali rasmi, huku wazalishaji wakitakiwa kusajili dawa zao kwanza kabla ya kuomba kibali cha kuyasemea kwa umma.










Post a Comment