POLISI PWANI YAFUNGIA LESENI MADEREVA WANANE, 55 WAFIKISHWA MAHAKAMANI
Madereva wanane wamefungiwa leseni huku wengine 55 wakifikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani kufuatia operesheni zilizofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ndani ya mwezi Mei 2026.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amesema jumla ya makosa 16,833 ya usalama barabarani yalibainika katika kipindi hicho.
Amefafanua wahusika walichukuliwa hatua za kisheria na kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani.
Morcase ameeleza katika operesheni nyingine, jeshi hilo liwakamata watuhumiwa 11 wa wizi wa mifugo na kufanikiwa kuokoa ng’ombe 28 waliokuwa wameibwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Ameongeza kuwa kesi 298 zilifikishwa mahakamani ndani ya kipindi hicho, huku kesi 128 zikisikilizwa na kukamilika.
Kwa mujibu wa Morcase, baadhi ya watuhumiwa wamehukumiwa vifungo vya miaka 30, miaka 37 na kifungo cha maisha kwa makosa mbalimbali yakiwemo ubakaji, kujeruhi na ulawiti.

Post a Comment