SERIKALI YAENDELEA KUWAWEZESHA WANAWAKE KUPATA MITAJI, MAFUNZO NA MASOKO
Serikali imeendelea kuimarisha juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa kupanua upatikanaji wa mitaji, mafunzo na masoko, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wao katika shughuli za uzalishaji mali na maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa Juni 17, 2026 bungeni Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Janeth Mahawanga, aliyehoji kuhusu mipango maalum ya Serikali ya kuwawezesha wanawake.
Akijibu swali hilo, Mahundi amesema Serikali imeweka mifumo mbalimbali ya uwezeshaji inayotekelezwa kupitia wizara za kisekta pamoja na mamlaka za serikali za mitaa, kwa lengo la kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi, kuongeza kipato na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi.
Ameeleza kuwa miongoni mwa mipango hiyo ni utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Jenga Kesho Yako (BBT) katika sekta za kilimo, mifugo na ufugaji nyuki,na katika sekta ya madini,kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linaendesha programu maalum zinazowawezesha wanawake kushiriki katika uchimbaji na biashara ya madini kwa kuwapatia mafunzo, maarifa na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za uwekezaji, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wao katika sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa.

Post a Comment