TASAC YATOA ELIMU YA HUDUMA ZA USAFIRI MAJINI KATIKA MAONESHO YA SABASABA 2026



Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri Baharini (TASAC) inaendelea kutumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutoa elimu kwa wananchi na wadau kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo katika kusimamia sekta ya usafiri majini nchini.

Kupitia banda lake lililopo katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, TASAC inatoa fursa kwa wananchi kupata maelezo kuhusu usimamizi wa biashara ya uwakala wa meli, masuala ya usalama na ulinzi wa usafiri majini, pamoja na uhifadhi wa mazingira ya bahari na maziwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazotumika.

Wananchi wanaotembelea banda hilo pia wanapata nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na wataalamu wa TASAC, kuuliza maswali kuhusu huduma zinazotolewa na kujifunza namna mamlaka hiyo inavyochangia maendeleo ya sekta ya usafiri majini na uchumi wa buluu nchini.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, ametembelea banda la TASAC leo Julai 1, 2026 na kupongeza jitihada za mamlaka hiyo katika kuendelea kusimamia kwa ufanisi biashara ya uwakala wa meli, usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira ya usafiri majini.

Maonesho ya Sabasaba, yaliyoanza rasmi Juni 28, 2026, yamewakutanisha washiriki kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali wakionesha bidhaa, huduma, ubunifu na fursa za biashara na uwekezaji.

TASAC inaendelea kuwakaribisha wananchi, wadau wa sekta ya usafiri majini na washiriki wote wa maonesho kutembelea banda lake ili kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na mchango wa mamlaka hiyo katika kujenga sekta ya usafiri majini iliyo salama, shindani na yenye tija kwa maendeleo ya uchumi wa taifa.









No comments