TFS YAWEKA NGUVU SEKTA YA MISITU NA NYUKI KUWA CHANZO CHA AJIRA
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeelekeza nguvu katika kuonesha namna sekta ya misitu na nyuki inavyoweza kuwa chanzo kikubwa cha ajira, kipato na uwekezaji kupitia bidhaa zilizoongezwa thamani na teknolojia mpya.
Akizungumza katika banda la Wizara ya Maliasili na Utalii, Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, DCC Emmanuel K. Wilfred, alisema taasisi hiyo imekuja na mkakati mpya wa kuwaonesha wananchi kuwa rasilimali za misitu zinaweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia bidhaa mbalimbali zinazotokana na mazao ya misitu na nyuki.
Alisema miongoni mwa vivutio vikubwa mwaka huu ni mbegu za miti migumu zinazowapa wananchi nafasi ya kuanzisha mashamba ya miti yenye thamani kubwa ya kibiashara, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji wa mbao na kupunguza utegemezi wa misitu ya asili.
Wilfred alisema TFS pia imewasilisha bidhaa mpya za asali zilizoongezwa thamani, ikiwemo asali zilizochanganywa na Royal Jelly, ambazo zimeandaliwa kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao ya nyuki na kuwapatia watumiaji bidhaa zenye manufaa zaidi kiafya na kibiashara.
Aidha, taasisi hiyo inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa kuonesha majiko ya kisasa yanayotumia kiwango kidogo cha umeme, yakilenga kupunguza matumizi ya mkaa na kuni sambamba na kulinda rasilimali za misitu na mazingira.
Mbali na maonesho ya bidhaa, wananchi wanaotembelea banda la TFS wanapata elimu kuhusu ufugaji wa nyuki, upandaji wa miti na fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya misitu, huku taasisi hiyo ikitoa wito kwa umma kutumia maonesho hayo kujifunza na kunufaika na fursa zinazopatikana.




Post a Comment