TANZANIA KUPANUA WIGO WA MASOKO YA UTALII KOREA KUSINI



WAZIRI  wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji mnamo Julai 22, 2026 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Jamhuri ya Korea (Korea Kusini) Mhe. Noel Kaganda.

  

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Mji Mkuu wa Jamhuri ya Korea wa Seoul, Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza moja ya jukumu muhimu la Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini ni kushiriki katika kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana Tanzania.


Amesema mkakati huo wa kutangaza vivutio vya utalii unalenga kuendelea kuifungua zaidi Tanzania Kimataifa na kupanua wigo wa masoko ya utalii kwa nchi za bara la Asia.

  

Mhe. Dkt. Kijaji ameeleza kuwa mbali na vivutio vya utalii katika hifadhi mbalimbali, Tanzania ina utajiri wa maeneo ya urithi na malikale ambayo yakitangazwa kimkakati yataongeza idadi kubwa ya wageni wanaoingia nchini ikiwa ni hatua na jitihada za kuhakikisha Tanzania inatimiza lengo la kufikia idadi ya watalii milioni 8 ifikapo mwaka 2030.

  

Waziri Dkt. Kijaji amewasili Korea Kusini kushiriki Mkutano wa 48 wa Kamati ya Urithi wa Dunia ulioanza Julai 19, 2026 na utaendelea hadi Julai 29, 2026 katika mji wa Busan nchini humo.

  

Kwa upande wake Balozi Kaganda ameahidi kufanya kazi bega kwa bega na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ili kubuni njia bora za kuitangaza Tanzania na vivutio vyake katika taifa hilo ambalo watu wake wanavutiwa zaidi na utalii wa utamaduni na mambo ya kale.




No comments