USHIRIKIANO WA WIZARA ZA FEDHA NA MALIASILI WAWEKEWA MSISITIZO KUKUZA UCHUMI KUPITIA UTALII
Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Wizara ya Fedha na Wizara ya Maliasili na Utalii katika jitihada za kuongeza mchango wa sekta ya utalii na maliasili kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Hatua hiyo imejidhihirisha kupitia kikao kilichowakutanisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, pamoja na wataalamu kutoka wizara hizo, kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili namna ya kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza mapato yanayotokana na utalii na maliasili, pamoja na kuboresha sera na mifumo itakayochochea ukuaji endelevu wa sekta hizo.
Walisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya wizara hizo ni msingi muhimu wa kutekeleza vipaumbele vya Serikali na kuhakikisha rasilimali za nchi zinatumika kwa ufanisi zaidi katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Serikali inaamini kuwa uratibu huo utaongeza mchango wa sekta ya utalii na maliasili katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwemo azma ya kujenga uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Elijah Mwandumbya pamoja na viongozi wa taasisi mbalimbali za uhifadhi na maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Benki Kuu na Wizara ya Maliasili na Utalii.








Post a Comment