DC KISARAWE AIPONGEZA TASAC KWA MCHANGO WAKE KATIKA ELIMU



Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Petro Magoti, amelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kazi nzuri inayofanya katika kutekeleza majukumu yake pamoja na mchango wake katika maendeleo ya jamii kupitia programu za Uwajibikaji wa Shirika kwa Jamii (CSR).


Mhe. Magoti ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la TASAC katika maonesho ya Tamasha la Kizimkazi  ambayo yanafanyika katika Viwanja vya maonesho Dimbani, kuanzia tarehe 12 na linatarajiwa kufungwa rasmi 14 Agosti12026.


Amesema TASAC imekuwa na mchango mkubwa katika kuunga mkono maendeleo ya elimu wilaya ya Kisarawe kupitia CSR, hatua ambayo imechangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi.


Aidha, Mhe. Magoti ameishukuru TASAC kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuimarisha sekta ya elimu na kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata mazingira bora ya kujifunzia.


TASAC inashiriki katika Tamasha la Kizimkazi 2026 ikiwa na lengo la kuwa karibu na wananchi na wadau, kutoa elimu kuhusu majukumu na huduma zake pamoja na kuongeza uelewa kuhusu usalama, ulinzi na ufanisi wa usafiri majini nchini.






No comments