NIRC YATANGAZA NEEMA KWA WAKULIMA NANE NANE
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), inaendelea na utekelezaji wa Mkakati mkubwa wa kuimarisha kilimo cha Umwagiliaji
nchini kwa kuzindua miradi mipya zaidi ya 30 katika mwaka wa fedha 2026/27, huku ikitarajia kuajiri maelfu ya vijana kupitia uchimbaji wa visima na usimamizi wa miundombinu ya Umwagiliaji.
Pia inalenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kufanikisha azma ya sekta ya kilimo kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika Viwanja vya Dr. John Malecela, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa amesema kwa kipindi cha miaka michache ya utekelezaji wa majukumu yake, tume imefanikiwa kuwa na wakandarasi 146 wanaotekeleza miradi mbalimbali ya Umwagiliaji, huku miradi 634 ikiwa katika hatua za usanifu.
Amesema lengo ni kuhakikisha mkulima anakuwa na uwezo wa kuzalisha kwa tija na kuacha kutegemea mvua.
Katika mpango huo, jumla ya pampu za kawaida (surface pumps) 1,000 zitatolewa ili kuwasaidia wakulima wa mbogamboga na matunda kuvuta maji kwa urahisi kutoka kwenye mito na mabonde, jambo ambalo litafanyika kwa njia salama isiyoharibu mazingira.
Sambamba na hilo, zaidi ya pampu 1,000 za kisasa zinazotumia nishati ya jua (solar pumps) zimenunuliwa maalum kwa ajili ya wakulima wa zao la parachichi.
Mpaka sasa, tayari visima 415 vimechimbwa huku lengo kuu likiwa ni kuchimba visima 67,000 ndani ya miaka nane ijayo.





Post a Comment