WANANCHI WANASHUKURU RAIS SAMIA KUFUTA HATI NA. 4873 YA SHAMBA LA MIFUGO LA KABIMITA- DC MPOGOLO.



Wananchi wa Bangulo na Pugu Stesheni,  wamemshukuru, Rais Dokta Samia Suluhu Hassan, kwa dhamira yake na upendo wa  kuridhia kufutwa kwa Hati Na. 4873 ya Wizara ya Mifugo, iliyokuwa ikilitambua eneo hilo kama Shamba la Mifugo la Kabimita, hatua inayofungua fursa kwa wananchi kupata haki ya kumiliki ardhi hiyo kihalali.


Akizungumza na wananchi wa Bangulo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema uamuzi huo wa Rais ni hatua kubwa yenye maana ya pekee kwa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi katika eneo hilo wakiwa na changamoto ya uhakika wa umiliki wa ardhi.


 Mpogolo amesema wananchi wanapaswa kumshukuru Rais Dkt. Samia  kwa uamuzi huo, ambao umeonesha dhamira yake ya kusikiliza kilio cha wananchi, kutatua changamoto zao na kuhakikisha wanapata fursa ya kutumia ardhi kama nyenzo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


“Kwa dhati kabisa, tunamshukuru Rais wetu,. Dkt. Samia . Uamuzi wake wa kufuta Hati Na. 4873 ya Wizara ya Mifugo, iliyokuwa ikifahamika kama Shamba la Mifugo la Kabimita, ni uamuzi mkubwa kwa wananchi wa Bangulo. Tunauona kama ishara ya upendo wake kwa wananchi na dhamira yake ya kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kumiliki ardhi yao kihalali,” amesema  Mpogolo.


Amesema hatua hiyo imeondoa kikwazo kikubwa na sasa wananchi wanapaswa kutumia fursa hiyo kwa kukamilisha taratibu za upimaji, urasimishaji na upatikanaji wa hati miliki ili waweze kuwa wamiliki halali wa ardhi wanayoishi.







No comments