BALOZI YAKUBU AIHIMIZA TBS KUWANIA NAFASI ZA KIMATAIFA KATIKA SEKTA YA VIWANGO
Ujumbe wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Othman Chande, umemtembelea Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Yakubu, katika Ubalozi wa Tanzania jijini Paris. Ujumbe huo pia ulimjumuisha Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Abdul Katunzi.
Wajumbe walimweleza Balozi Yakubu kuwa kupitia mkutano huo wamekutana na wadau muhimu wa TBS na kujifunza mbinu bora za kuratibu viwango vya bidhaa zinazozalishwa nchini Tanzania na zile zinazoingizwa nchini.
Balozi Yakubu ameipongeza TBS kwa mafanikio hayo na kuwahimiza wataalamu wa Tanzania katika sekta ya viwango kujiandaa kuwania nafasi za uongozi na uwakilishi ndani ya Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO) na taasisi za viwango za kikanda barani Afrika.
Amesema ushiriki wa wataalamu wa Tanzania katika nafasi hizo utaiwezesha nchi kutoa mchango mkubwa zaidi katika mijadala na maamuzi kuhusu viwango vya kimataifa. Pia utasaidia kuimarisha ulinzi wa walaji, ubora wa bidhaa, pamoja na uwezo wa wazalishaji wa Tanzania kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Ujumbe huo uko jijini Paris kushiriki mkutano wa Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO).
Post a Comment