MAGEREZA TANZANIA KUSHIRIKIANA NA INDONESIA KIMKAKATI
Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP) Jeremiah Yoram Katungu, amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko, katika Ofisi Ndogo ya Mkuu wa Jeshi la Magereza, Ukonga jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuanzisha ushirikiano kati ya taasisi hizo.
Katika mazungumzo hayo, CGP Katungu ameeleza maeneo mbalimbali yanayoweza kuwa msingi wa ushirikiano, ikiwemo kilimo cha kisasa, ufugaji, matumizi ya zana za kisasa za kilimo, elimu ya ufundi kwa wafungwa, kuwajengea uwezo Maafisa na Askari, urekebu na utengamanisho, pamoja na kubadilishana uzoefu kupitia ziara za taasisi hizo katika nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Balozi Tri Yogo Jatmiko amepongeza hatua hiyo na kueleza kuwa yuko tayari kuyafanyia kazi maeneo ya ushirikiano yaliyowasilishwa, ili yaweze kuleta tija kwa pande zote mbili. Aidha, amesema Indonesia na Tanzania tayari zina historia ya ushirikiano mzuri katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo, elimu na afya, huku akiahidi kushughulikia kwa haraka hatua za kuanzisha ushirikiano huo.

Post a Comment