MAFUNZO YA EMT YAIMARISHA UWEZO WA TAIFA KUKABILIANA NA DHARURA ZA AFYA


Mafunzo ya Timu ya Kitaifa ya Mwitikio wa Dharura za Afya (EMT) yanayoendelea mkoani Mwanza yameelezwa kuwa ni hatua muhimu katika kuongeza uwezo na utayari wa wataalamu wa afya kukabiliana na dharura na majanga, kutoa huduma za matibabu kwa wakati na kuokoa maisha ya wananchi.


Washiriki wa mafunzo hayo wameeleza leo Septemba 9, 2026 kuwa wamejengewa uwezo na kuongeza uelewa kuhusu kanuni, viwango na taratibu za uendeshaji wa Timu ya Mwitikio wa Dharura pamoja na namna ya kutoa huduma za afya katika mazingira yanayohitaji mwitikio wa haraka.


Kwa mujibu wa washiriki, mafunzo hayo yamewaongezea ujuzi wa kufanya maamuzi kwa haraka na kwa usahihi wakati wa dharura pamoja na kuwaandaa kwa ajili ya kutumwa katika maeneo yanayokumbwa na majanga au dharura za kiafya.


Aidha, wameeleza kuwa moja ya mambo muhimu waliyojifunza ni umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu ambapo wataalamu kutoka kada mbalimbali wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia mgawanyo wa majukumu, mawasiliano na uratibu wa pamoja. Ushirikiano huo unawezesha kutoa huduma zinazokidhi mahitaji mbalimbali ya wagonjwa na waathirika wakati wa majanga.


Washiriki hao wameongeza kuwa uwepo wa Timu ya Kitaifa ya Mwitikio wa Dharura yenye wataalamu walioandaliwa na wenye ujuzi unaohitajika ni muhimu katika kuhakikisha nchi inakuwa na uwezo wa kutoa huduma za matibabu kwa wakati pindi linapotokea janga au dharura kubwa ya afya. Timu hiyo inajumuisha wataalamu mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa na kada nyingine muhimu katika mwitikio wa dharura.


Kwa upande wao, washiriki wameeleza kuwa maarifa na ujuzi wanaoupata kupitia mafunzo hayo wataendelea kuutumia katika maeneo yao ya kazi na kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha mfumo wa huduma za dharura nchini.


Mafunzo hayo pia yameelezwa kuwa ni sehemu ya maandalizi ya kuimarisha utayari wa Taifa kabla ya kutokea kwa dharura, hatua inayolenga kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa majanga na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa wakati.







No comments