MAFUNZO YA TIMU YA KITAIFA YA MWITIKIO WA DHARURA YAMEINGIA SIKU YA NNE MKOANI MWANZA
Mafunzo ya Timu ya Kitaifa ya Mwitikio wa Dharura (EMT), yanayoendeshwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), yameingia siku ya nne leo, Septemba 10, 2026, mkoani Mwanza, huku washiriki wakijikita zaidi katika mafunzo kwa vitendo yanayolenga kuimarisha uwezo wa kutoa huduma salama na zenye ufanisi wakati wa dharura na majanga.
Mafunzo hayo yanawakutanisha watumishi wa afya kutoka hospitali za halmashauri na vituo vya afya vya mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Kigoma, ambao wanaendelea kujengewa uwezo katika maeneo mbalimbali muhimu ya mwitikio wa dharura.
Katika siku hii ya nne, washiriki wamejikita katika kujifunza na kufanya mazoezi ya namna ya kutoa huduma kwa waathirika wa dharura na majanga kwa kuzingatia uzito wa hali zao, pamoja na namna ya kupanga vipaumbele kwa waathirika na watoa huduma wakati wa tukio la dharura.
Aidha, washiriki wamefanya mazoezi ya vitendo kuhusu maandalizi, upatikanaji na usimamizi wa mahitaji muhimu wakati wa dharura, ikiwemo vifaa vya kujikinga binafsi (PPE), dawa, vifaa tiba na mahitaji mengine muhimu yanayohitajika ili kuhakikisha mwitikio unakuwa wa haraka, salama na wenye ufanisi.
Sehemu nyingine ya mafunzo imejikita katika upatikanaji wa maji salama na usafi wa mazingira, pamoja na namna ya kupanga na kusimamia vifaa, dawa na mahitaji muhimu katika mazingira ya dharura na majanga.
Kwa upande wa kinga na udhibiti wa maambukizi (IPC), washiriki wamefanya mazoezi ya vitendo yanayolenga kuimarisha usalama wa wagonjwa na watoa huduma. Mazoezi hayo yanahusisha usafi sahihi wa mikono, matumizi sahihi ya vifaa vya kujikinga pamoja na utunzaji na utupaji salama wa taka zinazozalishwa wakati wa utoaji wa huduma za afya.
Kwa ujumla, mafunzo ya siku ya nne yameweka msisitizo mkubwa kwenye kujifunza kwa vitendo, ili kuwawezesha washiriki kutumia maarifa na ujuzi walioupata katika mazingira halisi ya dharura na majanga, na hivyo kuimarisha uwezo wa timu za afya kutoa mwitikio wa haraka, salama na wenye ufanisi.

Post a Comment