MKURUGENZI MKUU WA TASAC ATEMBELEA WADAU WA SHIRIKA MKOANI MTWARA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, amefanya ziara ya kikazi mkoani Mtwara kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na wadau, kutathmini maendeleo ya huduma za usafiri majini na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Katika ziara hiyo, aliyoifanya tarehe 7 Septemba 2026, Bw. Salum alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na kukutana na Katibu Tawala wa Mkoa, Bi. Bahati Geuzye, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa. Bi. Geuzye aliishukuru TASAC kwa kuendelea kushirikiana na Mkoa huo na kuahidi kuimarisha mahusiano kwa manufaa ya maendeleo ya bandari na huduma za usafiri majini.
Mkurugenzi Mkuu pia alitembelea Bandari ya Mtwara na kukutana na Meneja wa Bandari, Bw. Ferdinand Nyathi, aliyemweleza kuhusu mafanikio na changamoto zinazoikabili bandari hiyo.
Miongoni mwa mafanikio ni ongezeko la mapato ya bandari kutoka wastani wa Shilingi bilioni 5 hadi takribani Shilingi bilioni 10 kwa mwezi. Aidha, Bandari ya Mtwara imeanza kuhudumia meli za mizigo mchanganyiko, hatua inayopanua wigo wa huduma na fursa za biashara. Hata hivyo, kupungua kwa meli za mafuta kumeendelea kuwa changamoto kwa bandari hiyo.
Ziara hiyo ilihitimishwa katika Bandari Kavu ya ISCON, ambapo Bw. Salum alikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kukutana na mwekezaji. Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia masharti ya kisheria na taratibu zinazotakiwa ili kukamilisha mchakato wa kupata leseni na kuanza shughuli kwa wakati. Pia alimpongeza mwekezaji kwa hatua zilizofikiwa na kuahidi ushirikiano wa TASAC.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Salum aliwahimiza wadau kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo inayotolewa na Serikali kupitia TASAC, ili kuhakikisha huduma za usafiri majini zinatolewa kwa ufanisi, ubora na usalama ili kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi ya Mtwara na Taifa kwa ujumla.
Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa TASAC wa kukutana na wadau na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kujadiliana njia bora za kuzitatua kwa lengo la kuboresha huduma za usafiri na uchukuzi majini nchini.


.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)


.jpeg)



Post a Comment