RAIS SAMIA AWATAKA WAKUU WA MIKOA KUWA WATUMISHI WA WANANCHI
ZANZIBAR:
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka Wakuu wa Mikoa walioteuliwa na viongozi wengine wa Serikali kutambua kuwa wao ni wawakilishi wa Rais katika maeneo yao ya kiutawala na kwamba wajibu wao mkuu ni kuwatumikia wananchi.
Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo katika Ikulu Ndogo ya Tunguu, Zanzibar, wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa mbalimbali pamoja na Katibu Tawala wa Mkoa walioteuliwa hivi karibuni.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Samia amewataka viongozi hao kuimarisha ukusanyaji wa mapato katika maeneo yao na kuhakikisha fedha za umma zinasimamiwa na kutumika kwa ufanisi, badala ya kutegemea kila jambo kutoka Serikali Kuu.
Aidha, amewataka kusimamia upangaji wa wafanyabiashara wadogo katika maeneo rasmi kwa kutumia njia za maelewano na kuepuka matumizi ya nguvu.
Rais Dkt. Samia pia ametoa maelekezo kwa viongozi hao kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri inawafikia vikundi vyenye uwezo wa kuzalisha matokeo chanya na kuchangia maendeleo ya wananchi.
Kuhusu ardhi, amewataka Wakuu wa Mikoa kusimamia matumizi bora ya ardhi kwa kuzingatia mipango miji ili kupunguza na hatimaye kumaliza migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
Vilevile, ameelekeza kila Mkoa kuendelea na maandalizi ya kukabiliana na mvua za El Nino, sambamba na kuhakikisha maeneo ya mikoa yanakuwa safi wakati wote.
Rais Dkt. Samia amesisitiza kuwa utekelezaji wa maelekezo hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuchochea maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Post a Comment