SERIKALI YAONGEZA FURSA ZA MAFUNZO YA UFUNDI STADI KWA WANAWAKE



Serikali imeeleza kuwa inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kuwapatia wanawake mafunzo ya ufundi stadi kwa lengo la kuwawezesha kuibua fursa za kibiashara, kujiajiri na kuongeza kipato.


Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Fatma Rembo, aliyehoji kuhusu mpango wa Serikali wa kuwapatia wanawake mafunzo ya ufundi stadi ili kuwawezesha kuibua fursa za kibiashara.


Naibu Waziri Mahundi amesema Serikali kupitia utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kisekta inaendelea kutoa fursa za mafunzo ya ufundi stadi kwa wanawake ili kuwawezesha kupata ujuzi unaoweza kuwasaidia katika shughuli za kiuchumi, ambapo miongoni mwa hatua zinazotekelezwa ni kupitia Mradi wa Uwezeshaji kupitia ujuzi unaolenga wasichana wenye umri wa miaka 18 hadi 35, ambapo hadi Juni 2026 jumla ya wasichana 1,051 walikuwa wamefikiwa na mradi huo.


Aidha, amesema kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Serikali inaendelea kutoa mafunzo ya vitendo kwa wanawake katika fani mbalimbali, ikiwemo ushonaji, utengenezaji wa bidhaa pamoja na matumizi ya teknolojia.


Aidha amesema Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Utambuzi na Urasimishaji Ujuzi, inayolenga kutambua na kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na hadi Juni 2026, jumla ya vijana 14,400, sawa na asilimia 18 ya lengo, kutoka mikoa 11 walikuwa wamesajiliwa katika programu hiyo inayolenga kuwafikia vijana 80,000 ifikapo Juni 2027.







No comments